Utoaji wa leseni na vibali

Kwa mujibu wa kifungu husika cha Sheria ya sekta ya tumbaku, Bodi ya Tumbaku Tanzania inaweza kutoa leseni na vibali vifuatavyo kwa watu au kampuni iliyosajiliwa:

 1. Leseni ya kununua tumbaku mbichi shambani;
 2. Leseni ya kuingiza tumbaku mbichi nchini;
 3. Leseni ya kusindika tumbaku;
 4. Leseni ya kununua tumbaku iliyosindikwa;
 5. Leseni ya kuuza tumbaku iliyosindikwa;
 6. Leseni ya kusafirisha tumbaku nje ya nchi;
 7. Kibali cha kuingiza tumbaku nchini; na
 8. Kibali cha kusafirisha tumbaku nje ya nchi.

Namna ya kuomba Leseni na Vibali

Kampuni au mtu ambaye anayetaka kununua, kuuza, kusindika, kuingiza au kusafirisha tumbaku nje ya nchi anapaswa kuomba leseni au / na kibali Bodi ya Tumbaku kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa kutoa leseni na vibali (ATMIS) kwa kutembelea https://atmis.kilimo.go.tz au kwa kutembelea tovuti ya Bodi na bonyeza linki mfumo wa vibali wa leseni.

Mahitaji kwa ajili ya kuomba leseni

Mwombaji wa leseni atatakiwa kutoa taarifa zifuatazo kwa Bodi ya Tumbaku:-

 1. Jina na anwani ya mwombaji;
 2. Ushahidi wa kusajiliwa na Bodi;
 3. Taarifa nyingine yoyote kama inaweza kuonekana kuwa muhimu.

Mambo yanayoweza kuifanya Bodi kukataa kutoa leseni kwa mwombaji

Bodi inaweza kukataa kutoa leseni kwa mwombaji ambaye:-

 1. Ameshindwa kuonyesha ushahidi wa uwezo wa kufanya biashara zinazohusiana na leseni anayoomba;
 2. Kwa mtizamo wa Bodi, mwombaji hawezi kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni;
 3. Anadaiwa na Bodi, mkuima, mnunuzi au msindikaji; au
 4. ameshindwa kuzingatia vigezo na masharti yanayohusiana na leseni iliyotolewa kwake katika msimu uliopita.

Kusimamishwa na kufutwa kwa leseni

 1. Bodi, kwa sababu maalumu zinazojulikana kwa mmiliki wa leseni iliyotolewa, inaweza kusimamisha au kufuta leseni.
 2. Mtu / kampuni, ambayo leseni yake imesimamishwa au kufutwa na Bodi, haitafanya miamala yoyote ya kibiashara inayohusina na leseni hiyo katika kipindi cha kusimamishwa au kufutwa..
 3. Mara tu mmiliki wa leseni atakapo rekebisha tatizo lililolazimisha kusimamishwa kwa leseni na baada ya kuisha kwa katazo lililowekwa, Bodi itasitisha kusimamishwa kwa leseni husika.