Kwa madhumuni ya ufuatiliaji wa mikataba ya kilimo, kusimamia ubora wa tumbaku, kusimamia chausindikaji wa uzalishaji wa bidhaa za tumbaku, kudhibiti uagizaji na usafirishaji wa tumbaku, kuanzisha msingi wa upangaji na kushughulika na suala lingine lolote linalohusiana na sekta ya tumbaku, Bodi ya tumbaku Tanzania ina mamlaka ya kusajili wakulima wote wa tumbaku nchini. Bodi inatoa vitambulisho kwa wakulima waliosajiliwa na hakuna ada ya usajili inayolipwa.

Sifa za kusajiliwa kama mkulima wa tumbaku

Mtu anastahili kusajili kama mkulima wa tumbaku kama ataithibitishia Bodi kuwa kwamba:

 1. ana nia ya dhati ya kuanza kulima tumbaku ndani ya kipindi cha miezi sita, kabla ya kipindi cha usajili kuisha kama inavyoelezwa katika kalenda ya shughuli za zao la tumbaku;
 2. ardhi ambayo tumbaku itapandwa ipo ndani ya ukanda wa kiikolojia uliotangazwa kufaa kwa ajili ya kulima tumbaku;
 3. ukubwa wa shamba ambalo tumbaku itapandwa si chini ya hekari moja.

Mahitaji kwa ajili ya kusajiliwa kama mkulima wa tumbaku

 1. jina la mkulima mwanachama na kama ni chama cha msingi au kikundi, majina ya wakulima binafsi;
 2. aina ya tumbaku itakayopandwa na maeneo yatakayolimwa katika mwaka huo wa maombi;
 3. mabani ya kukaushia tumbaku yaliyopo kwa kiasi cha tumbaku kilichokadiriwa kulimwa;
 4. kiasi cha zao, makisio ya uzalishaji, hifadhi ya pembejeo na nyongeza ya pembejeo zinazohitajika katika mwaka huo wa maombi;
 5. stoo za kuhifadhia tumbaku itakayolimwa;;
 6. vituo vya kuchambulia na kufungia tumbaku.

Kufuta usajili wa wakulima

 1. Bodi itamwondoa kwenye orodha mkulima yeyote wa tumbaku atakayeonekana kushindwa kukidhi vigezo na masharti ya usajili kama ilivyotolewa katika sheria na kanuni za tumbaku.
 2. Mkulima yeyote wa tumbaku ambaye ana mkataba wenye mikopo ataruhusiwa tu kufuta usajili wake baada ya kutoa taarifa miezi mitatu kabala ya nia yake ya kufanya hivyo.