Kwa kutambua haja ya kudhibiti uzalishaji, na kukuza maendeleo endelevu, Serikali ya Tanzania chini ya Sheria ya sekta ya Tumbaku Na. 24 ya 2001, ilianzisha Bodi ya Tumbaku Tanzania, kuchukua nafasi ya iliyokuwa Bodi ya Usindikaji wa Tumbaku na Masoko Tanzania (TTP & MB).

Sheria ya sekta ya tumbaku inalenga kuleta maendeleo yaliyokusudiwa ya sekta  ya tumbaku nchini. Majukumu mbalimbali ya Bodi yaliyoainishwa katika sheria ya udhibiti na ukuzaji wa sekta ni: -

  1. Kuishauri Serikali juu ya sera na mikakati ya kuboresha na kuendeleza sekta ya tumbaku nchini;

  2. Kuhamasisha maendeleo ya uzalishaji, na usindikaji wa tumbaku;

  3. Kuweka kanuni kwa ajili ya udhibiti wadudu waharibifu na magonjwa ya tumbaku;

  4. Kudhibiti na kuagiza hatua za uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuepuka uharibifu wa ardhi kupitia mpango wa upandaji miti wa lazima, na matumizi sahihi ya nishati ya kuni,

  5. Kusaidia moja kwa moja au kupitia uwezeshaji wa kifedha katika utafiti na maendeleo ya suala lolote linalohusiana na sekta ya tumbaku;

  6. Kusimamia na kudhibiti viwango vya ubora wa tumbaku;

  7. Kukusanya, kufanya uchambuzi, kutunza, kutumia na kusambaza taarifa mbalimbali zinazohusiana na sekta ya tumbaku;

  8. Kuweka sheria na kanuni zinazohusu taratibu za kilimo, masoko, usafirishaji, uuzaji wa tumbaku nje ya nchi  na uhifadhi wa tumbaku;

  9. Kuiwakilisha serikali katika mikutano ya kimataifa inayohusiana au kushughulika na tumbaku;

  10. Kuhamasisha na kuwezesha uundwaji wa vyama au mashirika mengine ya wadau katika sekta ndogo ya tumbaku (ambayo itaunda jukwaa la ushauri lililodhaminiwa na Bodi) na kuratibu shughuli zao.