Habari
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania afungua mafunzo ya ndani kwa watumishi wapya
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania Bw. Stanley Mnozya amefungua rasmi mafunzo maalum ya ndani kwa watumishi wapya wa Bodi, akisisitiza umuhimu wa kujenga nidhamu ya kazi, kuongeza tija na kutumia ubunifu katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo mjini Morogoro, Mkurugenzi Mkuu amesema Bodi inaendelea kutekeleza mkakati wake wa kuongeza tija katika usimamizi wa zao la tumbaku ili kuhakikisha mchango wake katika uchumi wa taifa unaendelea kuongezeka. Ameeleza kuwa mkakati huo unategemea nguvu kazi yenye weledi na inayofanya kazi kwa bidii bila kuridhika na mafanikio madogo.
Amesisitiza kuwa watumishi wapya wanatarajiwa kuwa sehemu ya mabadiliko ndani ya taasisi na kuwa wabunifu katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya tumbaku. Amesema ubunifu ndio nguzo itakayowezesha Bodi kuongeza ufanisi na kuendana na mahitaji ya sasa ya usimamizi wa mazao ya biashara.
Aidha, ameweka wazi kuwa Serikali imeweka lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la tumbaku nchini hadi kufikia tani laki 3 ifikapo mwaka 2030. Amesema Bodi ina wajibu wa kuhakikisha mazingira ya uzalishaji, masoko na huduma kwa wakulima yanaboreshwa ili kufikia malengo hayo kwa wakati.
Mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwajengea uwezo watumishi wapya na kuwawezesha kuelewa majukumu, miongozo na misingi ya utendaji ndani ya Bodi ya Tumbaku Tanzania.