Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Bodi ya Tumbaku Tanzania

Habari


Watendaji wa masoko ya tumbaku wamaliza mafunzo kwa mafanikio, Masharti mapya ya masoko yatangazwa


Mbeya, 25 Aprili 2025 — Semina na mkutano wa siku tatu wa Watendaji wa Masoko ya Tumbaku kwa mwaka 2025 umehitimishwa kwa mafanikio makubwa. Akifunga mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania Bw. Stanley N. Mnozya amewashukuru washiriki kwa kujifunza kwa bidii na kusisitiza matumizi ya elimu waliyoipata kuboresha sekta ya tumbaku nchini.

Katika hotuba yake, ameeleza kuwa makampuni ya ununuzi wa tumbaku yanatakiwa kukamilisha masharti yote kabla ya kupewa leseni, yakiwemo malipo kwa wakulima na ushuru husika. Kati ya makampuni 19 yaliyosajiliwa kwa msimu wa 2024/2025, ni makampuni 8 pekee yaliyokamilisha masharti hayo hadi sasa. Bodi imetoa muda wa mwisho hadi tarehe 27 Aprili 2025 kwa makampuni hayo kukamilisha taratibu, vinginevyo hatua mbadala zitachukuliwa kuhakikisha wakulima wanauza tumbaku yao bila matatizo.

Bodi imezielekeza timu za ununuzi kufika kwa wakati kwenye vituo vya kununulia tumbaku, na kuonya kuwa wakulima watakaochanganya ngulai kwenye tumbaku zao na kukiuka taratibu za masoko watatozwa faini ya TZS 500,000. Aidha, kampuni zitakazoshindwa kuwalipa wakulima ndani ya siku 14 baada ya mauzo hazitaruhusiwa kuendelea na ununuzi katika msimu wa masoko wa 2025/2026.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi amesisitiza vikao vya tathmini ya masoko kufanyika kila baada ya wiki mbili katika kila Mkoa wa Kitumbaku ili kushughulikia changamoto zinazojitokeza mapema. Serikali pia imeagiza kutotolewa kwa leseni ya ununuzi kwa Kampuni ya Voedsel, huku hatua zikichukuliwa kuhakikisha wakulima walioingia mikataba na kampuni hiyo wanalipwa na kupata wanunuzi mbadala.

Mwisho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi amewahimiza washiriki wa semina kuendeleza uadilifu, kuepuka vitendo vya rushwa na kushirikiana kwa lengo la kukuza Sekta ya Tumbaku nchini.