Habari
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania waaswa kuzingatia wajibu na majukumu ya wajumbe wa mabaraza ya wafanyakazi mahali pa kazi

Mbeya, 26 Aprili 2025 - Wajumbe wa baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania wameaswa kuzingatia wajibu na majukumu ya wajumbe wa mabaraza ya wafanyakazi mahali pa kazi.
Hayo yamesemwa na Afisa Kazi Bi. Christina Matage kutoka Idara ya Kazi Mkoa wa Morogoro wakati akiwasilisha mada juu ya wajibu na majukumu ya wajumbe wa baraza la wafanyakazi kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania katika ukumbi wa GR City Hotel jijini Mbeya.
Bi. Christina Matage amebainisha kuwa mada hii ina lenga kuwajenga na kuwaimarisha wajumbe wa baraza juu ya majukumu yao ndani ya baraza na kutoa maelezo ya nini kinajadiliwa katika baraza la Wafanyakazi.
Baraza la Wafanyakazi ni chombo cha mawasiliano na ushauri ambacho viongozi na wafanyakazi hukaa pamoja na kuzungumzia mpango kazi na uchumi wa taasisi yao na kutathimini ufanisi na tija baada ya kupanga na kutekeleza mipango ya taasisi.
Aidha, Bi. Christina Matage amewasisitiza wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mablimbali inayosimamia sera ya ushirikishwaji wa wafanyakazi (baraza la wafanyakazi). Amezitaja sheria, kanuni na miongozo hiyo ambayo ni: Sheria ya utumishi wa Umma Na. 8 ya 2002, kanuni ya 2003 (kanuni mpya GN 444 za mwaka 2022), Sheria ya Majadiliano katika Utumishi wa Umma Na. 19 ya 2003, kanuni ya 2005, Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini Na. 6 ya 2004, Kanuni za 2007 (Sura 366 marejeo ya mwaka 2019), Sheria ya Taasisi za kazi Na. 7 ya 2004, kanuni za 2007. (Sura 300 marejeo ya mwaka 2019), Agizo la Rais Na.1 la 1970 (Angalizo), Mikataba mbalimbali ya shirika la kazi Duniani (ILO) ambayo Tanzania imeridhia, Sheria inayo anzisha shirika, taasisi, wakala au idara na Mkataba wa kuunda baraza.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Bodi ya Tumbaku Tanzania ambaye pia ndiye Mkurugezi Mkuu wa Bodi Bw. Stanley N. Mnozya amemshukuru Bi. Christina Matage kwa mada yake nzuri kwa wajumbe wa baraza na kuahidi kuwa baraza la wafanyakazi la Bodi ya Tumbaku Tanzania litatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia mabaraza ya wafanyakazi mahali pa kazi.