Habari
Bodi ya Tumbaku yatangaza bei ya wastani ya tumbaku kwa msimu wa kilimo 2025–2026
Bodi ya Tumbaku Tanzania imetangaza bei ya wastani ya tumbaku kwa msimu wa kilimo 2025–2026 kuwa ni dola za Marekani 1.95 kwa kilo.
Tangazo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku, Bw. Stanley N. Mnozya, kufuatia kikao cha Halmashauri ya Tumbaku kilichofanyika tarehe 21 Januari 2026.
Bw. Mnozya amesema kuwa uamuzi wa bei hiyo umetokana na tathmini ya kina ya hali ya soko la tumbaku duniani, ubora wa tumbaku inayozalishwa nchini, pamoja na gharama za uzalishaji zinazowakabili wakulima. Lengo kuu ni kuhakikisha wakulima wananufaika na bei ya nzuri huku sekta ya tumbaku ikiendelea kuwa na ushindani katika soko la kimataifa.
Kikao hicho kilihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya tumbaku, wakiwemo wakulima, wanunuzi na wawakilishi wa serikali, ambao kwa pamoja walijadili mwenendo wa soko na changamoto zilizopo katika uzalishaji wa zao hilo.
Bodi ya Tumbaku imewahimiza wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo cha tumbaku ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao, hali itakayowawezesha kunufaika zaidi na bei elekezi iliyotangazwa. Aidha, wanunuzi wametakiwa kuzingatia bei hiyo wakati wa ununuzi wa tumbaku msimu huu.
Sekta ya tumbaku inaendelea kuwa chanzo muhimu cha kipato kwa wakulima na mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa, hivyo Bodi imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha maslahi ya pande zote yanalindwa.