Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Bodi ya Tumbaku Tanzania

Habari


Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania ashiriki Uzinduzi wa masoko na Upangaji bei ya tumbaku Zimbabwe kwa Msimu wa 2025/2026


Harare, Zimbabwe – Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Bw. Stanley Mnozya, ameshiriki katika uzinduzi wa masoko na upangaji wa bei ya tumbaku kwa msimu wa mwaka 2025/2026 uliofanyika nchini Zimbabwe.

Akizungumza baada ya kushiriki uzinduzi huo, Bw. Mnozya alieleza kufurahishwa na maandalizi mazuri yaliyofanywa na mamlaka husika nchini humo, hususan namna wakulima walivyopatiwa taarifa mapema kuhusu hali ya soko ili waweze kujiandaa na mabadiliko ya bei. Alieleza kuwa hatua hiyo imewasaidia wakulima kuelewa mapema sababu za kushuka kwa bei ya tumbaku katika soko la dunia, kunakosababishwa na ongezeko la uzalishaji wa zao hilo.

Bw. Mnozya alifafanua kuwa katika masoko yaliyofanyika tarehe 4 Machi 2026, bei ya tumbaku ilishuka kwa wastani wa dola moja kwa kila daraja. Pamoja na hali hiyo, wakulima wameaswa kupokea changamoto ya msimu huu kwa kuzingatia zaidi ubora wa tumbaku, kuongeza tija katika uzalishaji na kuhakikisha wanauza tumbaku yao kwa wakati.

Aliongeza kuwa hali hiyo ya kushuka kwa bei si ya Zimbabwe pekee, bali pia inaathiri nchi nyingine zinazozalisha tumbaku ikiwemo Tanzania.

“Ninafahamu kuwa hata Tanzania hatupo salama kutokana na anguko hilo la bei. Hata hivyo, napenda kuwataarifu wakulima kuwa pamoja na changamoto hiyo, Bodi ya Tumbaku itahakikisha haki inatendeka kwa pande zote mbili, yaani mkulima na mnunuzi,” alisema Bw. Mnozya.

Aidha, alitoa wito kwa wanunuzi wa tumbaku kuhakikisha wanazingatia haki katika mchakato wa ununuzi na kuepuka kuwadhulumu wakulima kwa kisingizio cha kushuka kwa bei ya tumbaku duniani.

“Kamwe asiwepo mnunuzi hata mmoja atakayejificha kwenye kichaka cha anguko la bei na kumdhulumu mkulima. Iwapo itabainika, Bodi haitasita kuchukua hatua kali za kisheria,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Bw. Mnozya aliwakumbusha wanunuzi kuwa bei inayotangazwa ni bei elekezi. Hivyo, mnunuzi hatakiwi kununua tumbaku kwa bei iliyo chini ya bei hiyo, lakini anaruhusiwa kutoa bei ya juu zaidi.
Kutokana na hilo, Bodi ya Tumbaku imezitaka kampuni zinazojihusisha na ununuzi wa tumbaku kufanya ununuzi kwa ushindani kwa kutoa bei nzuri zaidi kwa wakulima, zaidi ya bei elekezi, ili kuongeza tija na motisha kwa wazalishaji wa zao hilo nchini.