Kwa madhumuni ya kufuatilia mikataba ya kilimo, kudhibiti ubora wa tumbaku, kudhibiti usindikaji wa tumbaku na utengenezaji wa bidhaa za tumbaku, kudhibiti uingizaji na usafirishaji wa tumbaku nje ya nchi, kuanzisha msingi wa kupanga na kushughulika na jambo lingine lolote muhimu katika tasnia ya tumbaku, Bodi ya Tumbaku Tanzania imepewa jukumu la kusajili wakulima wote wa tumbaku nchini. Bodi hutoa vitabulisho kwa wakulima waliosajiliwa na hakuna ada ya usajili inayolipwa kwa bodi.
Sifa za kusajiliwa kama mkulima wa tumbaku
Mtu yeyote anastahili kusajiliwa kama mkulima wa tumbaku ikiwa ataithibitishia Bodi kwamba:
- Ana nia ya dhati ya kuanza kulima tumbaku ndani ya kipindi cha miezi sita, kabla ya kipindi cha usajili kuisha kama inavyoelezwa katika kalenda ya shughuli za zao la tumbaku;
- Ardhi ambayo tumbaku itapandwa ipo ndani ya ukanda wa kiikolojia uliotangazwa kufaa kwa ajili ya kulima tumbaku;
- Ukubwa wa shamba ambalo tumbaku itapandwa si chini ya hekari moja.
Mahitaji kwa ajili ya kusajiliwa kama mkulima wa tumbaku
- jina la mkulima mwanachama na kama ni chama cha msingi au kikundi, majina ya mkulima mmoja mmoja;
- aina ya tumbaku itakayopandwa na maeneo yatakayolimwa katika mwaka huo wa kuomba kusajiliwa;
- mabani ya kukaushia tumbaku yaliyopo kwa kiasi cha tumbaku kilichokadiriwa kuzalishwa;
- kiasi cha zao, makisio ya uzalishaji, hifadhi ya pembejeo na nyongeza ya pembejeo zinazohitajika katika mwaka huo wa maombi;
- stoo za kuhifadhia tumbaku itakayolimwa; na
- vituo vya kuchambulia na kufungia tumbaku.
Kufuta Usajili wa Wakulima
- Bodi itamwondoa kwenye orodha mkulima yeyote wa tumbaku atakayeonekana kushindwa kukidhi vigezo na masharti ya usajili kama inavyoelekeza katika sheria na kanuni za tasnia tumbaku.
- Mkulima yeyote wa tumbaku ambaye ana mkataba wenye mikopo ataruhusiwa tu kufutiwa usajili wake baada ya kutoa taarifa miezi mitatu kabala ya nia yake ya kufanya hivyo.