Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bodi ya Tumbaku Tanzania

Sisi ni Nani

Bodi ya Tumbaku Tanzania ni chombo cha udhibiti wa zao la tumbaku kilichoanzishwa chini ya sheria ya sekta ya tumbaku Na. 24 ya 2001 (kama ilivyorekebishwa na sheria ya mazao (marekebisho mchanganyiko) Na. 20 ya 2009). Majukumu makuu ya udhibiti ya Bodi kama yalivyoelezwa katika sehemu ya tano (5) ya sheria ya tumbaku ni:-

  1. Utungaji, utekelezaji na usimamizi wa Sera, Miongozo na Viwango kwa lengo la kudhibiti na kuboresha utendaji wa tasnia ya tumbaku nchini Tanzania;
  2. Kutoa ushauri kwa Waziri anayehusika na Kilimo na Serikali kwa ujumla juu ya masuala yote yanayohusiana na Sekta ya tumbaku; na
  3. Uhamasishaji na uendelezaji wa mazingira mazuri kwa ajili ya ufanisi na ushindani kwa wadau wote katika sekta ya tumbaku.

Dira

Kuwa bora katika utoaji wa huduma za udhibiti, ushauri na ukuzaji wa sekta ya tumbaku.

Dhamira

Kutoa huduma kwa wakati na ubora kwa wakulima na wafanyabiashara wa tumbaku katika suala la usajili, ushauri wa kitaalam na uwezeshaji wa mchango wa sekta binafsi katika sekta ya tumbaku kwa ukuaji bora na endelevu kwa manufaa ya sekta na nchi.

Shughuli Kuu

Shughuli kuu za Bodi ni kukuza, kuendeleza na kudhibiti tasnia ya tumbaku nchini Tanzania.

Historia ya Bodi ya Tumbaku

Historia ya Bodi ya Tumbaku inarudi miaka ya 1960 wakati Serikali ilipoanzisha Bodi ya Tumbaku ya Tanganyika. Mnamo mwaka 1970 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzisha Mamlaka ya Tumbaku ya Tanzania (TAT). TAT ilibadilishwa mnamo 1984 kuwa Bodi ya Usindikaji wa Tumbaku na Masoko Tanzania.

Mnamo mwaka 1993 Bodi ya Usindikaji wa Tumbaku na Masoko Tanzania ilirekebishwa tena kuwa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) kufuatia ubinafsishaji wa sekta ya tumbaku ambayo ilifikia kilele mnamo 1997 wakati shughuli za Bodi ya Tumbaku zilipofadhiliwa na Serikali. Bodi ya sasa ni matokeo ya Sheria ya Sekta ya Tumbaku Na.24 ya 2001, na marekebisho yake ya mwaka 2009.

Mamlaka ya Bodi

Katika kutekeleza majukumu yake, Bodi ya Tumbaku Tanzania imepewa mamlaka ya kisheria yafuatayo:

  1. Kufuatilia utendaji wa sekta binafsi ambayo jukumu lake la msingi ni la kibiashara kuhakikisha inafanya kazi kulingana na sheria ya tasnia ya tumbaku na sera zingine za nchi zinazofanana.
  2. Kukuza ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na ya Umma kwa utekelezaji wa majukumu ya pamoja.
  3. Kuandaa mapendekezo ya kitaalam kwa Serikali juu ya masuala ya sera ya tumbaku ili kuinua mchango wa tasnia kwa maendeleo ya nchi.

Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Sekta ya Tumbaku No.24 ya 2001, Bodi ina mamlaka yafuatao: -

  1. Kusajili au kutoa leseni kwa wakulima, wauzaji na wasindikaji wa tumbaku.
  2. Kutoa leseni kwa wanunuzi, wauzaji na wasindikaji wa tumbaku.
  3. Kutoa leseni kwa ajili ya kusafirisha au kuingiza tumbaku nje au ndani ya Tanzania.
  4. Kuteua wakaguzi kwa ajili ya ukaguzi wa maeneo ya tumbaku, na kitu chochote ambacho kinaweza kukaguliwa kwa lengo la utekelezaji bora wa masharti ya sheria.